Advert


java

Connectify - Turn Your PC into a Wi-Fi Hotspot. Install now!

Wednesday, May 3, 2017

MBEYA CITY YAWASHANGAA YANGA KUTEMBEZA BAKULI

Kuna ujumbe nilikutana nao katika mitandao ya kijamii siku za hivi karibuni. Ukiusoma unafurahisha sana lakini umebeba ujumbe mzito sana.
Unasema wakati mwanamuziki Diamond Platnum amefanya hafla kubwa ya kuzindua biashara yake inayofahamika kama CHIBU PERFUME ambayo inauzwa shilingi laki moja na elfu tano (105000) kuna klabu kubwa hapa  nchini zimeshindwa kuweka utaratibu mzuri wa kujipatia hata 20000 kutokana na mauzo ya jezi za mastaa wao.

Maisha ndivyo yalivyo, kupanga ni  kuchagua. Diamond ameamua kuisimamisha Brand yake na wengine wameona kuwarudia wananchi wawachangie ndiyo maisha wanayostahili.

Diamond huyu ameamua kuingia kwenye ulimwengu mwingine tofauti na ule wa muziki. Ulimwengu wa kibiashara ambao unahitaji watu makini wanaoweza kuifanya biashara kusimama bila kuyumba. Sio kazi rahisi kama unavyoweza kufikiri unapoitazama ukiwa nje. Hata kama atakuwa anakutana na changamoto za hapa na pale ila kitu alichokifanya ni kikubwa sana.

Ubunifu wa aina hii ndio unaompa Cristiano Ronaldo jeuri ya kumiliki ndege binafsi na kuiishi dunia vile atakavyo.

Alishindwa Ngassa, Msuva nae licha ya kuwa na uhakika wa kukutana na mashabiki zaidi ya milioni kumi kwa mwaka bado anahisi hili ni kubwa sana kwake.

Kwa mazingira ya soka letu inawezekana suala hili likawa gumu kwa wachezaji wetu lakini hawana budi kubadilika maana dunia nayo imebadilika. Ni aibu sana mchezaji wa kizazi cha dunia ya leo kuishi katika dunia aliyoishi Sunday Manara au Athuman Machupa.

Sawa inawezekana wachezaji wanahofia ukubwa wa Brand zao lakini vipi kuhusu klabu nazo? Bado nazo zinahofia kuhusu ukubwa wa Brand?

Ukitafakari vizuri utakubaliaana na mimi hiki sio kikwazo kwa klabu zenye idadi kubwa ya mashabiki kama hizi za Kariakoo. Kama umeweza kuamini watu wanaweza kukuchangia fedha bure unashindwaje kuwatumia watu hao hao kuwa sehemu ya mtaji au soko lako?

Mpaka hapo unaweza kuamini na mimi tatizo kubwa linaloukwamisha mpira wetu kupiga hatua ni watu wanaouongoza mpira wenyewe.

Rasilimali watu ni kitu muhimu sana katika mustakabali wa maendeleo ya sekta yoyote. Ulishawahi kujiuliza kuwa Yanga wangeweza kuachwa na ndege nchini Algeria kama wangekuwa na mtaalamu wa masuala ya Logistics? Bila ya kuwa na watu sahihi unaweza kuwa na kila kitu lakini bado usifanikiwe.

Nairejea kauli ya Zeben Hernandez aliyekuwa kocha wa Azam fc wakati anaondoka alisema uwekezaji mkubwa bila watu sahihi ni sawa na bure.

Wanasema unapoona mdogo anamzidi mkubwa kwa busara na maarifa basi huitaji kufikiri sana kugundua hapo kuna tatizo.

Mbeya City anazidi kuyafanya tuliyotarajia kuyaona yakifanywa na kaka zake siku nyingi zilizopita.
Licha ya uchanga wao lakini wanaamini tayari nembo yao ni Brand inayoweza kuwapa fedha kutoka kwa wadhamini na kuwaondoa katika kundi la omba omba.

Mbeya City wametangaza rasmi wamesaini mkataba wa udhamini na kampuni ya vifaa vya michezo ya Sports Master.

Udhamini huo utaifanya kampuni hiyo kuwa mtengenezaji na msambazaji mkuu wa vifaa vyote vya michezo vitakavyokuwa vinatumiwa na klabu ya Mbeya City katika kipindi chote cha miaka miwili ya mkataba huo. 

Hii ina maana kuwa mbali na timu hiyo kunufaika na vifaa vya michezo vitakavyokuwa vikitengenezwa na kampuni hiyo pia itakuwa imeongeza chanzo kingine cha mapato kwa sababu kampuni ya Sports Master watalazimika kuilipa Mbeya City kutokana na nembo yao kuonekana kwenye jezi ya klabu hiyo.

Hii ni aina mojawapo kati ya zile aina za udhamini wa kwenye jezi ambapo makampuni mbalimbali ya Marekani na Ulaya kama Adidas na Nike huzilipa klabu kubwa fedha nyingi kwa ajili ya udhamini huu.

Kwa sasa Manchester united ndio wanaoongoza kwa kuingiza kiasi kikubwa cha fedha kutokana na udhamini huo ambao wanaingiza kiasi cha Pauni milioni 75 kwa mwaka za Adidas wakifuatiwa na Chelsea watakaokuwa wakiingiza kiasi cha Pauni milioni 60 za Nike kwa mwaka kuanzia msimu ujao.

Ni hatua kubwa sana waliyopiga kama klabu kwa sababu wanaweza kuwa wameonyesha mfano kwa kuwa klabu ya kwanza Tanzania kufanya hivyo. Ndio wameweza. 

Unafikiri Mbeya City wana nini cha kuwapa shavu kama hili zaidi ya viongozi makini?

Ndugu zetu wa Kariakoo wanalitambua hili?

Yupo mmoja anavaa jezi zinazotengenezwa na makampuni ya Nike na Kelme na mwingine akivaa zilizotengenezwa na kampuni ya Uhlsport.

Nisaidie hapa Je, klabu zinanufaika na chochote kutoka kwenye makampuni hayo kwa kuzitangaza nembo zao?

Jibu la swali hili ni jepesi sana, kama kinapatikana basi kinaishia tusikokujua mimi na wewe.

Mbeya City wameonekana kuwa makini sana kwa namna wanavyoingia katika masuala haya ya kibiashara.

Ukiachana na aina hii ya udhamini wa jezi ambao klabu hunufaika kutokana na kutangaza makampuni ya utengenezaji wa vifaa vya michezo, pia kuna aina nyingine ya udhamini kupitia kwenye jezi ambapo klabu inaweza kuwa na wadhamini kadhaa kati ya mmoja au zaidi ambao bidhaa zao zitatangazwa kwenye jezi ya timu husika.

Mdhamini mkuu ndio hukaa sehemu ya mbele au sehemu ya tumbo wakati wale wadogo wakikaa nyuma mgongoni au kwenye fito za mikono.

Kwa aina hii ya udhamini Mbey city wanadhaminiwa na Bin Slum kupitia bidhaa yake ya RB Batteries ambayo nembo yake huonekana mbele ya jezi za timu hiyo. Pia Coca Cola ambao wanaidhamini timu hiyo kupitia jezi yao ambapo nembo yao huonekana kifuani kwa size ndogo juu ya nembo kubwa ya mdhamini mkuu.

Wanachokipata Mbeya City kutokana na ubunifu wao wa kutengeneza vyanzo vya mapato unawasaidia kuendesha timu bila ya kuwa na matatizo ya hapa na pale  ambayo yamekuwa ni sehemu ya maisha ya kawaida kwa klabu zetu.

Licha ya udogo wa klabu yao lakini wamefanikiwa kuitumia nembo yao hiyo ndogo kunufaika nayo. Nawaza hapa ingekuwaje kama wao ndio wangekuwa na Brand kama zile za klabu fulani?

Wanahitaji nini zaidi ya kuwashangaa wasiojua ukubwa na thamani ya Brand za klabu zao? Sina budi kuwapongeza Mbeya city katika hili.

Ifike hatua tufikiri kutengeneza fedha za kuendeshea klabu zetu kutokana na nembo za klabu zenyewe. Bila kubadilika hatutaisha kutembeza bakuli kuomba misaada.

Klabu inahitaji kuwa na watu sahihi kila sekta ili kuendana na usasa. Hili linawahusu watu wa idara ya masoko ambao wanaweza kuhakikisha wanatengeneza mazingira mazuri ya kuwavutia wawekezaji na wadhamini ndani ya klabu.

Hivi kweli kwa ukubwa wa Simba, leo hii wanavaa jezi plain isiyokuwa na hata nembo ya mdhamini yeyote?
Najiuliza hapa wadhamini ndio wanakosekana au tatizo ni wao kutokujua thamani ya jezi yao.

Mbeya city hawana la kufanya zaidi ya kuendelea kuwashangaa na michango yao pamoja na madeni yao wanayoendelea kuyatengeneza kila siku maana unaweza kushangaa mmoja anamcheka mwenzie kwa kuamua kutembeza bakuli wakati wao wanaendesha timu kwa mikopo.

No comments:

Post a Comment