Advert


java

Connectify - Turn Your PC into a Wi-Fi Hotspot. Install now!

Wednesday, March 19, 2014

Kutoka bungeni....

HOTUMA YA JAJI WARIOBA YAFUNIKA

 

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba jana aliliteka Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma, alipowasilisha Rasimu ya Katiba na kushangiliwa katika maeneo mengi nyeti na kupigiwa kelele katika vipengele vichache vya uraia na ardhi. 

Katika hotuba yake ya maneno 14,112 iliyosomwa kwa saa 3:34, Jaji Warioba aliweka wazi maoni ya wananchi yaliyomo katika ibara 271 za Rasimu hiyo, ukiwamo muundo wa Muungano wa Serikali Tatu – Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Zanzibar.
Mwanasheria huyo alijenga hoja zake zilizoisaidia Tume yake kufikia hitimisho la muundo huo, kwamba ilizingatia maoni ya wananchi, yakiwamo ya mabaraza ya katiba ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Ofisi ya Waziri Mkuu na Baraza la Wawakilishi Zanzibar ambayo ama moja kwa moja au kwa tafsiri yalipendekeza muundo wa Serikali Tatu.
Alisema tume hiyo ililazimika kupendekeza muundo huo kutokana na kero, hoja na malalamiko yaliyotolewa na pande mbili za Muungano wakati tume hiyo ikukusanya maoni, pamoja na hoja zilizotolewa miaka ya nyuma na tume mbalimbali.
“Suala la muundo wa Serikali Tatu limechukua nafasi kubwa katika mjadala tangu tume ilipozindua Rasimu ya Kwanza ya Katiba. Mjadala wa muundo wa muungano umekuwa mkubwa kiasi cha kufunika mapendekezo mengine yaliyomo katika Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano,” alisema Warioba katika hotuba yake ya aya 191.
Huku akishangiliwa na baadhi ya wajumbe, Jaji Warioba alisema kwa tahmini ya tume hiyo, muundo wa Serikali mbili hauwezi kubaki kwa hali ya sasa.
“Muungano wa Serikali mbili waliotuachia waasisi siyo uliopo sasa. Umebadilishwa mara nyingi, wakati mwingine bila ya kufanya mabadiliko kwenye Katiba. Waasisi walituachia Muungano wa nchi moja yenye Serikali mbili na siyo nchi mbili zenye Serikali mbili,” alisema.
Alisema muundo wa Serikali mbili unaweza kubaki tu ikiwa orodha ya mambo ya muungano haitapunguzwa bali itaongezwa na isipokuwa hivyo Serikali ya Muungano itabaki na rasilimali na mambo ya Tanzania Bara tu.
“Katika hali hiyo, pande zote mbili zitaendelea kulalamika. Kwa upande mmoja, Zanzibar itaendelea kulalamika kwamba Tanzania Bara imevaa koti la Muungano kwa faida yake na kwa upande mwingine, Tanzania Bara itaendelea kulalamika kwamba mambo yasiyo ya Muungano ya Tanzania Bara na rasilimali zake, ndizo zimekuwa Muungano,” alisema.
Warioba alishangiliwa tena na baadhi ya wajumbe aliposema: “Muundo wa Serikali Tatu haupunguzi uimara wa Muungano na muungano huo ni wa nchi mbili kwa manufaa ya wananchi, “Faida kubwa iliyopatikana katika miaka hamsini iliyopita ni kuungana kwa wananchi.”
Waliotoa maoni
Kuhusu idadi ya waliotoa maoni, alisema watu wengi waliotoa maoni kuhusu Muungano walijikita katika muundo wake kama njia ya kuondoa kero,” alisema.

Alifafanua kwamba Tanzania Bara wananchi zaidi ya 39,000 walitoa maoni kuhusu muungano na kati ya hao, 27,000 walizungumzia muundo wake.
Kwa Zanzibar, wananchi karibu wote waliotoa maoni walijikita kwenye suala la Muungano na kwamba kati ya watu 38,000 waliotoa maoni kuhusu Muungano, 19,000 walitoa maoni kuhusu muundo wake.
“Wananchi waliotoa maoni kuhusu muundo wa Muungano kwa upande wa Tanzania Bara, asilimia 13 walipendelea Serikali moja, asilimia 24 Serikali mbili na asilimia 61 waliendekeza Serikali Tatu” alisema na kuongeza;
Utafiti wa Tume
Alisema kuwa baada ya kuchanganua sababu mbalimbali zilizotolewa na makundi mbalimbali tume hiyo ilianza kufanya utafiti wa kina kuhusu muundo wa muungano na matatizo yake tangu ulipoundwa Aprili 26, 1964, na kutaja tume zilizopendekeza Serikiali tatu.
Alizitaja tume ya Jaji Francis Nyalali ya mwaka 1993, kundi la Wabunge 55 kutoka Tanzania Bara (G 55) waliopeleka bungeni hoja ya kuundwa kwa Serikali ya Tanganyika na Tume ya Jaji Kisanga.
Changamoto Serikali Tatu
Kuhusu Serikali Tatu ambao chama tawala (CCM), kimekuwa kinaupinga kwa udi na uvumba, Jaji Warioba alisema muundo huo utakuwa na changamoto zake, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa gharama ingawa hazitakuwa kubwa kama inavyofikiriwa.
“Gharama kubwa kwa shughuli za Muungano ni katika eneo la ulinzi na usalama, yaani jeshi la wananchi, polisi, usalama wa taifa na mambo ya nje. Gharama hizo hazibadiliki, zinabaki zile zile bila kujali kama ni muundo wa Serikali mbili au Serikali tatu,” alisema.
Alisema tangu Muungano uundwe, Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar zimekuwa zikiongeza wizara, mikoa, wilaya na taasisi mbalimbali za kiutawala ili kuleta ufanisi na hivyo kuongeza matumizi ya Serikali.
“Tume imependekeza kodi ya bidhaa iwe ya Muungano, pia mapato yasiyo ya kodi, mikopo na michango ya nchi washirika. Ushuru wa bidhaa utakidhi sehemu kubwa ya gharama za muungano,” alisema na kuongeza:
“Kwa upande wa matatizo ya kiutendaji, tume imependekeza muundo wa Serikali tatu ujengwe kwenye misingi minne ya utendaji – muungano wa hiyari, ushirikiano, mshikamano na kutegemeana.