MAGAVANA WA ADB KUKUTANA ARUSHA
Mkutano Mkuu wa Magavana wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), unatarajia kufanyika jijini Arusha kuanzia Mei 30 hadi Juni Mosi, mwakani. Hayo yalisemwa jana na Mwakilishi Mkazi wa AFDB, Dk. Tonia Kandiero, wakati akizungumza na Rais Jakaya Kikwete, Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya kwenda kujitambulisha.
Rais Kikwete akiwa na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Tonia Kandiero, aliyemtembelea jana na kufanya mazungumzo Ikulu jijini Dar es Salaam.
Taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana ilieleza kuwa Dk. Kandiero, alisema kuwa pamoja na mambo mengine, amekwenda Ikulu kumueleza rasmi Rais Kikwete kuhusu mkutano huo wa magavana hao ambao hata hivyo hakufafanua yatakayojadiliwa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, AfDB ni moja ya wahisani wakubwa wa Tanzania kwa kutoa misaada kwenye miradi ya maendeleo na hasa sekta za barabara, kilimo, maji na nishati. (Chanzo: Nipashe)
No comments:
Post a Comment