Maharusi wakiwa katika honeymoon.
Nimekuwa nafuatilia jinsi desturi ya kuchangia na kufanya sherehe kubwa
inavyozidi kushika kasi, ikipelekea ule wigo wa kuomba michango kupanuka
kiasi kwamba sasa hata mtu ambaye jina lako halijui vizuri anaweza kukuomba
mchango.
Aidha michango na sherehe hizi zimekuwa mzigo mkubwa sana kwa baadhi ya
watu, ikiwa ni pamoja na wale wenye kipato kidogo wanaochangiwa na
kulazimika kulipa michango hiyo kwa miaka mingi. Je, wajua kuwa kuna familia
ambazo zimefikia kulazimisha ndugu wauze mashamba au mifugo mtaji ili kupata
fedha za kuchangia sherehe?. Je, wajua kuwa kuna watu ambao zaidi ya nusu ya
kipato chao wanatumia kuchangia sherehe na huku wakishindwa kulipia huduma
muhimu kama shule, matibabu, lishe, nk. Na kuwa wakati mwingine wewe au mimi
(au wengine kama mimi na wewe) ndio wenyeviti na makatibu wa sherehe hiyo?.
Na ni sisi tunaoona fahari ya kutumia milioni 30 au zaidi kwenye sherehe
usiku mmoja?
Kuna kijana mmoja jamaa yetu juzi juzi alipata shule Australia akawa
anatafuta mchango wa dola 5,000 aende. Alipata 2,000 na amwekwama kwenda.
Mwaka kesho akisema anaoa tutamchangia milioni 15-20!!!. Hii si hadithi, ni
ukweli, na ni kielelezo cha ulimbukeni tuliofikia.
Siku za karibuni nimetambua kuwa kuna kundi kubwa tu linasikitishwa na huu
mwenendo, na hata kutambua kuwa tunaweza kuwa tunaandikiwa dhambi kubwa (na
hukumu yatusubiri) kwa jinsi wengi wetu tunashindwa kusaidia mambo ya msingi
lakini tunakuwa wepesi kutoa kwenye sherehe. Wengi wanaamini kuwa
tumeshatumbukia kwenye lindi la mazoea ambapo hatuwezi kujitoa mpaka upepo
uje ubadilike wenyewe!.
Mimi nafikiri wasomi tuna jukumu muhimu la kuwa chachu ya mabadiliko pale
ambapo mazoea yenye madhara yanavuka mipaka na kuweza hata kuwa chanzo cha
ufukara na kuviza maendeleo.
Ili kubadilisha hili jambo, lazima tuanzie mahali. Mimi napendeleza na
kuanza kutekeleza. Kuanzia Januari 2011, nitapunguza michango ninayotoa.
Nitatoa tu kwa mtu wa karibu sana, na nitachanga kidogo. Usishangae
nikakuchangia 20,000/= kama ulitegemea 50,000/= kwa mfano. Kuanzia July
2011, nitaacha kabisa kuchangia sherehe. Badala yake nitakuwa nachangia
elimu pale ambapo mzazi hayupo au mhusika kweli hana uwezo na pia
nitachangia miradi mingine ya jamii na maendeleo.
Je waniunga mkono? Kama ndiyo sambaza huu ujumbe kwa mtandao wako.