RAIS KIKWETE AZUNGUMZIA KUHUSU MAAFA YA GONGO LA MBOTO
Ndugu Wananchi,
Kama mjuavyo, jana usiku jiji la Dar es Salaam lilipata mtikisiko mkubwa kutokana na milipuko ya mabomu iliyokuwa inatokea katika ghala kuu la Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania lililoko Gongolamboto katika viunga vya Dar es Salaam.
Milipuko hiyo imesababisha maghala 23 kuteketea kabisa na majengo kadhaa ya shughuli mbalimbali hapo kikosini kuharibika kwa viwango mbalimbali. Mabweni mawili ya kuishi wanajeshi nayo yaliteketea. Aidha, risasi nyingi, mabomu mengi, silaha na magari kadhaa nayo yameharibiwa na mengine kuteketea. Jeshi letu na nchi yetu imepata hasara kubwa sana.
Katika maafa haya makubwa kwa taifa letu, raia nao wameathirika kwa namna mbalimbali. Nyumba kadhaa za kuishi na majengo ya huduma za jamii nayo yameharibiwa na mabomu yaliyoangukia humo. Zipo ambazo zimeungua kabisa na zipo zilizopata uharibifu mkubwa na zipo zilizopata uharibifu wa viwango vya chini.
Lakini baya zaidi, katika mlipuko huo, ndugu zetu 20 wamepoteza maisha na wengine zaidi wamejeruhiwa kwa aina na viwango mbalimbali. Baadhi yao walifika katika hospitali za Amana, Temeke na Muhimbili na kupatiwa matibabu. Wengine wameruhusiwa na wengine wapatao 135 bado wamelazwa. Idadi kamili hupanda na kushuka kutegemea na kupokelewa na kuruhusiwa kwa majeruhi.
Ndugu Wananchi,
Hakika taifa limepata hasara kubwa kwa ndugu zetu kufariki na kujeruhiwa. Napenda kutumia nafasi hii kwa uchungu mkubwa kuelezea masikitiko yangu na taifa kwa ndugu zetu waliopoteza maisha wakati ambapo taifa lilikuwa bado linauhitaji sana mchango wao.
Naomba ndugu wa marehemu wapokee mkono wa rambirambi kutoka kwangu na kupitia kwangu kutoka kwa Watanzania wenzetu wote. Tuwaombee kwa Mwenyezi Mungu marehemu wetu wapate mapumziko mema. Amin.
Aidha, kwa niaba yangu na ya Watanzania wenzangu wote, nawapa pole nyingi ndugu zetu wote waliojeruhiwa na kupata mshituko kutokana na milipuko ya mabomu iliyotokea jana usiku. Tunazidi kuwaombea wapone upesi ili waendelee na kazi zao za kujenga taifa pamoja na kujiletea maendeleo yao binafsi.
Leo asubuhi na baadae mchana nilitembelea eneo la tukio kule Gongolamboto na kuwatembelea wagonjwa katika hospitali za Amana, Temeke na Muhimbili. Nimeona madhara na hasara tuliyoipata pale Gongolamboto. Nimewaona na kuwafariji wagonjwa wetu. Nimezungumza na madaktari na wauguzi katika hospitali hizo. Nimewashukuru na kuwapongeza kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya usiku kucha ya kuwahudumia na kuokoa maisha ya ndugu zetu hao. Nimewatia moyo na kuwataka waendelee kuwahudumia vyema.
Ndugu Wananchi,
Napenda pia kutumia nafasi hii kuwapongeza viongozi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na wa Bohari Kuu ya Madawa kwa kuhakikisha kuwa dawa na vifaa vya tiba vinapatikana kwa urahisi na kwa wakati, Hali hiyo ndiyo iliyosaidia kuokoa maisha na kuwapunguzia machugu ndugu zetu waliojeruhiwa.
Baraza la Usalama
Ndugu Wananchi,
Leo alasiri mpaka usiku huu, tulikuwa na mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Taifa. Hiki ndicho chombo cha juu cha kumshauri Rais kuhusu masuala yahusuyo usalama wa taifa letu. Kwa uzito na unyeti wa tukio, niliamua kuitisha mkutano wa Baraza hilo mara baada ya maafa hayo kutokea.
Katika mkutano wetu, tumelitafakari kwa kina tukio hili na mambo mbalimbali yanayotokana na kuhusiana nalo. Baraza limeazimia kama ifuatavyo:
1. Tumesikitishwa sana na tukio hili na hasa vifo vilivyotokea na majeraha yaliyowapata ndugu zetu wengi. Baraza limetoa rambirambi kwa ndugu na jamaa wa marehemu. Aidha, tunawapa pole wale wote waliojeruhiwa na kuwaombea kwa Mola wapone upesi.
2. Kuhusu waliopoteza maisha, tumeamua kuwa, Serikali igharamie mazishi ya marehemu wetu hao popote ndugu watakapoamua wakazikwe. Baadae ndugu wa marehemu wapewe kifuta machozi.
3. Kuhusu waliojeruhiwa tumeamua kuwa Serikali igharamie matibabu yao. Baadae watakapotoka hospitali walipwe kifuta machozi kwa ulemavu walioupata.
4. Kamati ya Maafa ya Mkoa imeagizwa kushirikiana na Kitengo cha Maafa cha Taifa kilichopo Ofisi ya Waziri Mkuu kuwahudumia wananchi waliopoteza makazi yao au waliolazimika kuyakimbia makazi yao kwa nia ya kuokoa maisha yao. Ihakikishwe kuwa kwa haraka wanapatiwa makazi ya muda pamoja na huduma za malazi, chakula, maji, afya na usafi wa mazingira.
5. Aidha, Kamati ya Maafa ya Mkoa imeelekezwa kutengeneza taratibu nzuri zitakazohakikisha kuwa mapema iwezekanavyo, wananchi hao wanarejea makwao ili waendelee na shughuli zao za kawaida hasa sasa ambapo hatari ya milipuko katika maghala ya Gongolamboto haipo tena.
6. Baraza la Usalama limelipongeza Jeshi la Ulinzi kwa uamuzi wake wa haraka wa kuwatuma wahandisi wa medani kufanya kazi ya kutafuta, kutambua na kuyakusanya mabomu yote yaliyoangukia katika maeneo ya raia kwa nia ya baadae kuyaharibu.
7. Tunawaomba wananchi watoe ushirikiano wa hali ya juu kwa Jeshi kwa kuwapa taarifa wanapoyaona mabomu katika maeneo yo yote. Na, jambo kubwa zaidi tunawakumbusha wananchi kutii maelekezo ya Jeshi ya kutokuyagusa au kuchezea mabomu au hata vipande vipande vya mabomu vilivyodondoka katika maeneo yao.
8. Baraza la Usalama la Taifa, limeagiza Kamati ya Maafa ya Mkoa wa Dar es Salaam na Kitengo cha Maafa cha Taifa wazitambue mapema iwezekanavyo nyumba zilizoharibiwa, wenye nyumba na kuhakikisha kuwa matayarisho husika yanafanyika ikiwa ni pamoja na uthamini ili walipwe fidia wanayostahili bila kuchelewa.
9. Vile vile Kamati ya Maafa ya Mkoa imeagizwa kufanya yafuatayo:
(a) Kushirikiana na Jeshi la Polisi kuwatafuta watoto waliopotea na kuwaunganisha na familia zao.
(b) Kuongoza, kuratibu na kusimamia utekelezaji wa masuala yote yahusuyo waliofariki, waliojeruhiwa na waliohama makazi yao, na huduma zao stahiki.
10. Baraza la Usalama limetoa pole nyingi kwa Mkuu wa Majeshi, Maafisa na Askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa maafa makubwa yaliyowakuta na hasara waliyoipata kwa milipuko ya mabomu iliyotokea katika Ghala Kuu la Jeshi, Gongolamboto.
11. Baraza pia limelipongeza Jeshi kwa juhudi kubwa ilizofanya kuzima moto huo, hivyo kuweza kunusuru baadhi ya maghala, zana na vifaa vingine visiteketezwe na moto.
12. Baraza limeagiza Jeshi lifanye uchunguzi wake wa ndani wa chanzo cha tukio hili kama Sheria ya Ulinzi wa Taifa inavyoagiza. Aidha, imetaka vyombo vingine vya ulinzi na usalama visaidie katika uchunguzi huo.
13. Baraza la Usalama limeamua kuwa, Serikali ya Tanzania iombe nchi rafiki zisaidie katika uchunguzi wa chanzo cha tukio hili na kushauri namna bora zaidi ya kuimarisha usalama na uhifadhi wa mabomu na risasi katika maghala ya Jeshi letu kote nchini.
14. Mwisho, Baraza la Usalama wa Taifa linawaomba wananchi waliohama warejee kwenye makazo yao kwani kipindi cha hatari ya mabomu kulipuka kimekwishapita. Tunaomba na kusisitiza wajiepushe kuchezea mabomu yaliyodondoka katika maeneo yao ambayo bado hayajaondolewa.
Ndugu Wananchi Wenzangu;
Hili ni janga ambalo pamoja na kusikitisha linaleta uchungu hasa pale inapotokea miaka miwili tu baada ya janga la Mbagala. Machungu yenu ndiyo machungu yangu na ndiyo ya viongozi wote Wakuu wa Nchi yetu ambao ndiyo Wajumbe wa Baraza la Usalama la Taifa. Naomba tuwe watulivu katika wakati huu mgumu.
Napenda kuwahakikishia kuwa tumeamua kulishughulikia tatizo lenyewe na athari zake sasa na siku za usoni kwa uthabiti mkubwa. Naomba tuendelee kuwa na imani na Jeshi letu, viongozi wake na wanajeshi wetu wote. Tuwaunge mkono na kuwapa ushirikiano sasa na siku za usoni.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa kunisikiliza.