Advert


java

Connectify - Turn Your PC into a Wi-Fi Hotspot. Install now!

Tuesday, June 30, 2015

WALIMU WANYANYASWA KISHIRIKINA BUNDA

MBUNGE wa Jimbo la Mwibara, Kangi Lugola amelazimika kukatisha vikao vya Bunge vinavyoendelea mjini Dodoma kwenda jimboni kwake, kijiji cha Nambaza, kata na tarafa ya Nansimo, wilaya ya Bunda mkoani Mara kushughulikia adha wanayoipata walimu wa shule ya msingi kijijini hapo wanaofanyiwa vitendo vya kishirikina, kudhalilishwa na kuteswa kishirikina na kulazimika kuomba uhamisho wakafundishe shule nyingine maeneo ya mbali na jimbo hilo.

Walimu wa shule hiyo ya msingi Nambaza wanadai usiku wakiwa wamelala wanaingiliwa na wachawi ambao wamekuwa wakiwanyoa nywele sehemu za siri, kuwafanyia vitendo vya ngono, kuwalawiti na kuwaibia mali na fedha kishirikina.

Aidha walimu hao wanadai kwamba, mbali na vitendo hivyo vya kuingiliwa kimwili, kulawitiwa, kunyolewa nywele sehemu za siri, kuibiwa mali na fedha kishirikina, pia wamekuwa wakikuta mikojo, ugali na samaki ukiwa umefunikwa na shuka kitandani, hali ambayo imewafanya washindwe kufundisha na kuomba wahamishwe katika shule hiyo.

Mwalimu Joyce Maugo ambaye ni mkongwe kidogo katika shule hiyo, kwa masikitiko huku akibubujikwa na machozi alisema, walimu wa shule hiyo wako hatarini kwa vitendo vya kishirikina wanavyofanyiwa, alisema mmoja wa walimu wenzake, msichana mdogo na mdogo kimaumbile aliingiliwa kimwili kishirikina mpaka kazimia.

Alisema, asubuhi alipoitwa kwenda kushuhudia yaliyomkuta mwalimu huyo mwenzake,  alikuta mambo ya aibu amefanyiwa mwalimu huyo, alikuwa hawezi kutembea, sehemu zake za siri zikiwa zimeharibiwa vibaya, kitanda kikiwa kimevurugwa hovyo hovyo, kikiwa na kinyesi, damu na mikojo kibao!

Bi. Joyce alisema mwalimu wa kiume Pasco Mayamba akiwa amefunga milango na madilisha ya chumba chake, asubuhi alipoamka alikuta madirisha na milango iko wazi, kitanda kimejaa mkojo, kitandani kwake ndani ya shuka alilojifunika kukiwa na bonge la ugali, kipande cha mnofu wa sangara na mchuzi mwingi.

Alisema, wakati fulani wakila chakula usiku, ghafla chakula kinabadilika, kama ulikuwa wali na nyama unakuwa ugali na dagaa au mboga za majani hali ambayo alisema ni ya mateso, adha na manyanyaso makubwa wanayoyapata nakuomba wahurumiwe, kama kuna makosa wamewafanyia wawaambie wawaombe msamaha ili wasiendelee kuwatesa na kuwanyima raha na amani kimaisha.

Mwalimu Lucy alisema, mbali na adha hizo watu hao wanawaibia fedha, vitambulisho, kadi za benki na mali nyingine, lakini pia wakati mwingine wanakuta mkojo na kinyesi katika madebe ya unga na chungu cha mboga vitendo ambavyo vinawanyima morari ya kazi na ari ya kuendelea kufundisha shule hiyo.

Kwa sasa mwalimu Lucy alisema watu hao wanahisaidia haja kubwa madarasani na kuwapa kibarua walimu na wanafunzi kuzoa kinyesi madarasani karibia kila siku na kuwasihi viongozi na wanakijiji wa kijiji hicho waliowema kuchukuwa hatua dhidi ya madhira hayo kwa walimu.

Akizungumza na majira jana akiwa mjini Bunda, mbunge Kangi alisema vitendo vya kishirikina wanavyofanyiwa walimu hao ambao ni wageni,  waliopelekwa shuleni hapo hivi karibu siyo vya kufumbiwa macho, ni vya kukemewa vikali na wahusika wakibainika wachukuliwe hatua kali kwani, mbali na madhara wanayoyapata walimu hao kwa kuingiliwa kimwili bila ridhaa yao na watu wasiowajua wala kuwaona,  pia vinawadhalilisha na vinalenga kudidimiza maendeleo ya elimu katika jimbo lake.

Kangi alisema,  amelazimika kwenda kijijini Nambaza kulishughulikia tatizo hilo ambapo leo Jumatatu, Juni 29, 2015 atafanya mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji hicho ili kutafuta ufumbuzi na dawa ya tatizo hilo ili likomeshwe na lisitokee tena.

Wananchi wa kijiji hicho katika mkutano wao wa hadhara walioufanya hivi karibuni waliwabaini kwa kuwapigia kura baadhi ya wanakijiji hicho kuwa ni wahusika wakuu katika kuwafanyia vitendo hivyo vya kishirikina walimu hao, kiongozi na kinara wa mch ezo huo mchafu akitajwa mmoja wa viongozi kijijini hapo anayeishi eneo jirani na shule hiyo.

Wanakijiji wa kijiji hicho waliazimia washukiwa hao wahame haraka kijijini hapo kabla hawajachukua sheria mkononi wakidai vitendo wanavyo vifanya mbali na kuvunja sheria vitasababisha shule yao ikose walimu wa kuwafundisha watoto wao hali ambayo  inaweza kusababisha kijiji kukosa wasomi na kuwa kijiji cha wahuni na vibaka.

Kuhusu maamuzi ya wanakijiji hao ya kuwataka wakazi wenzao, wanaowatuhumu kwa ushirikina kuhama kijiji, mbunge Kangi alisema, atayaheshimu maamuzi yao na kwamba kabla wananchi hawajafikia hatua ya kuchukua sheria mkononi atawashauri watu hao wahame kijiji hicho haraka.

Mkuu wa wilaya ya Bunda, Joshua Milumbe aliliambia majira kwamba, vitendo hivyo hawezi kuvivumilia, ni vitendo vya udhalilishaji, asivyoweza kuvifumbia macho lazima achukue hatua.

Mkuu wa wilaya Milumbe alisema, atakwenda Nambaza kuzungumza na wananchi wa kijiji hicho na kwa mamlaka aliyonayo kwa mujibu wa sheria atachukua hatua kali dhidi ya watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo vya kihuni akisisitiza ataheshimu maamuzi ya wananchi.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Bunda Bi. Lucy Msofe alisema,  amesikitishwa sana na vitendo hivyo wanavyofanyiwa walimu hao wenye umri mdogo na wadogo kwa maumbile akidai ni ukatili wa hali ya juu wanaofanyiwa walimu hao.

Bi. Msofe alisema, tayari amelazimika kumuhamisha mwalimu mmoja wa kike ambaye alifika kwake akiwa na hali mbaya kutokana na alivyofanyiwa na watu hao na kuongeza kwamba, endapo hali hiyo itaendelea atalazimika kuwahamisha walimu katika shule hiyo awapeleke katika shule wanayowahitaji,kuwaheshimu na kuwathamini kwani uenda shule ya msingi Nambaza hawahitajiki.

Alisema hayuko tayari kuendelea kushuhudia watoto wa watu wakiendelea kuteseka, kunyanyasika, kudhalilishwa na kufanyiwa unyama kiasi hicho akadai atawahamisha kama vitendo hivyo havitakomeshwa.